SERIKALI KUPITIA NFRA KANDA YA SHINYANGA IMETOA MSAADA BURE WA MAHINDI TANI KUMI KWA WANANCHI WALIOATHIRIKA NA MAJITOPE

by Radio Faraja

Serikali kupitia wakala wa taifa wa hifadhi ya chakula NFRA Kanda ya Shinyanga imetoa msaada wa bure wa mahindi tani kumi kwa wananchi walioathirika na majitope ya Mgodi wa Almasi wa Williamson Mwadui.

Msaada huo umetolewa Novemba 23,2022 ambao pia umekabidhiwa kwa wananchi hao na Mbunge wa viti maalum kupitia chama cha mapinduzi CCM Mkoa wa Shinyanga Lucy Mayenga.

Akizungumza mwakilishi wa NFRA Revocatus Bisama kwa niaba ya meneja wa NFRA kanda ya Shinyanga amesema tani tano zimeshafikishwa kwa waathirika na tani tano zitatolewa kwa awamu nyingine.

“Tulizungukia huku tukiwa na Mbunge Lucy Mayenga tukaona hali halisi ilivyo hivyo Mbunge akaiomba serikali iweze kuwasaidia wananchi walioathirika na kupoteza makazi yao” Bisama Alisema.

” serikali kupitia wakala wa taifa wa hifadhi ya chakula kanda ya shinyanga ikatoa msaada wa mahindi tani kumi sawa na gunia 200, na leo tumeleta tani tano sawa na gunia 100, kwaajili ya kuwasaidia waathirika wa Mwadui” Alisema Bisama.

Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Shinyanga Lucy Mayenga amesema msaada huo umetolewa baada ya kuiomba serikali iweze kuwasaidia wananchi waliokutwa  na adha hiyo.

” Haya mahindi ilikuwa nitoe pesa zangu mfukoni lakini baada ya kuongea na Waziri wa Kilimo Hussen Bashe akanizuia akasema serikali itatoa ili kuwasaidia wananchi” Alisema Lucy Mayenga.

“Tuishukuru serikali pamoja na NFRA ambao wanahifadhi mahindi pamoja na uongozi wote wamekuwa tayari lakini zaidi tumshukuru Rais Samia, na kwamba mtapata mgao wenu, lakini mumtangulize Mungu kwa kila jambo” Lucy Mayenga alisema.

Kwa upande wake Afisa Mahusiano katika Mgodi wa Almasi wa Williamson Mwadui WDL Bernard Mihayo amesema Mgodi umeendelea kuweka mikakati mbalimbali na kwamba unaendelea kuwahudumia wananchi wote walioathiriwa na tope.

“Kinachoendelea katika mgodi huu tunafanya marekebisho mbalimbali kuzuia madhara yasiendelee kusamba, pia kwa kushirikiana na Halmashauri ya Kishapu tunawatafutia mashamba mbadala kwaajili ya kilimo” Alisema mihayo.

“Pia tutafuta ardhi kwaajili ya kuwajengea nyumba lakini kwa sasa wapate sehemu za kupanga na kampuni italipia kodi kwa miezi sita, tutaendelea kutoa msaada mingine kama chakula, matibabu na kuhahikisha watoto wao wanasoma vizuri” Alisema Mihayo

Baadhi ya wananchi hao wameishukuru serikali kuendelea kutatua changamoto zao hususani kuwaletea msaada wa  mahindi.

“Tunaishukuru serikali kwa kutuletea msaada wa mahindi mahindi ambayo yatatusaidia kwenda kuanzia maisha maana vitu vyetu vyote viliharibika” Walisema wananchi.

Novemba 7,2022 kingo za Bwawa la tope katika Mgodi wa Mwadui unaomilikiwa na Kampuni ya Petra Diamonds zilibomoka na tope kuvamia makazi ya wananchi katika kijiji cha Ng’wanh’olo kata ya   Mwadui Luhumbo hivyo kusababisha uharibifu.

mwakilishi wa NFRA Revocatus Bisama kwa niaba ya meneja wa NFRA kanda ya Shinyanga
Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Shinyanga Lucy Mayenga
Afisa Mahusiano katika Mgodi wa Almasi wa Williamson Mwadui WDL Bernard Mihayo

Related Posts

Leave a Comment